Mbinu Kumi(10) Za
Kuwafanya Wateja Waendelee Kufanya Biashara Na Wewe.
Kazi kubwa sana unayohitaji
kufanya baada ya kumpata mteja ni kuhakikisha anaendelea kuwa wako, yaani
anaendelea kufanya biashara na wewe.
Wafanyabiashara wengi wamekuwa
wakitumia nguvu kubwa kuwafikisha wateja kwenye biashara zao, lakini wateja
wanapofika na kupata huduma huondoka na wengi kutokurudi tena.
Ni rahisi sana kumuuzia mteja
ambaye ulishamuuzia awali, kuliko kumuuzia mteja mpya. Hivyo kama ukiweza
kuiendesha biashara yako vizuri, wateja ambao wananunua kwako watakuwa wateja
wako wa kudumu.
Zifuatazo ni mbinu kumi
unazotakiwa kuanza kuzitumia leo kwenye biashara yako ili kuhakikisha wateja
wako wanaendelea kufanya biashara na wewe.
1.
Tekeleza ulichoahidi.
Kama umemtangazia mteja kwamba
akija kwenye biashara yako atapata kitu fulani, basi hakikisha anapata kitu
hiko. Hakuna kitu ambacho watu hawapendi kama kudanganywa. Mteja anapoona
kwamba amedanganywa hatorudi tena kwenye biashara yako na utakuwa umemkosa
milele. Hakikisha unatimiza ulichomwahidi mteja wako.
2.
Ahidi kikubwa na pitiliza(overpromise and overdeliver)
Najua hapa unaweza usielewe kwa
sababu ulichozoea ni kuahidi kidogo na kupitiliza(underpromise and
overdeliver). Hii ilikuwa unafanya kazi zamani, ila kwa sasa, haifanyi kazi
tena. Kwa sababu kama wewe unaahidi kidogo, wenzako wanaahidi kikubwa na
wanafanyia kazi. Hivyo kitu pekee cha kuhakikisha unawabakisha wateja ni
kuwaahidi makubwa na kuyapitiliza hayo. Kama umejitoa kweli kwenye biashara
yako, hili halitakushinda.
3.
Imarisha mawasiliano yako na wateja wako.
Ni muhimu sana uwe na
mawasiliano na wateja wako. Bila ya kujali ni biashara gani unafanya, kuna na
mfumo w akupata namba za simu, au barua pepe za wateja wako. Mata kwa mara
watumie ujumbe ukiwatakia heri na wakati mwingine kuwajulisha bidhaa au huduma
mpya zilizopo kwenye biashara yako.
4.
Fanyia kazi malalamiko ya wateja haraka.
Wateja wanapokuwa na
malalamiko, yafanyie kazi haraka sana. Usisubiri mpaka yawe makubwa kiasi cha
kuwafanya watafute mahali pengine wanakoweza kufanya biashara bila ya matatizo
wanayopata kwako.
5. Toa
huduma bora ambazo mteja hawezi kupata popote.
Huduma kwa wateja, mteja
amepokelewaje, ameelezwaje kuhusiana na bidhaa au huduma anayohitaji, maswali
yake yamejibiwaje, hivi ni vitu vinavyoonekana vidogo sana ila vina maana kubwa
sana kwa wateja wa biashara yako. hakikisha wateja wako wanapata huduma ambazo
zitawafanya wajisikie ufahari.
6.
Wakumbuke wateja waliopotea.
Kama biashara yako imekuwepo
kwa muda, kuna wateja waliokuwepo awali ila kwa sasa hawapo tena. Kuna wateja
ulikuwa unafanya nao biashara zamani, ila kwa sasa huwaoni tena kwenye biashara
yako. ni vyema kuwatafuta na kujua kwa sasa biashara wanafanya na nani na ni
kitu gani limewafanya hawaji tena kwako.
7.
Muuzie mteja baada ya kumuuzia.
Mara nyingi mteja atakuja kwako
akitaka kitu fulani, lakini pia anaweza kuwa anataka vingine zaidi ya
alichofuata hapo. Ni jukumu lako kujua mahitaji haya yote ya mteja wako na
kuyafanyia kazi. Usiishie kumuuzia mteja kitu kimoja pekee, hakikisha kila
anachohitaji ambacho kipo kwenye biashara yako, unampatia. Ataendelea kuja
kwako kwa sababu anajua mahitaji yake yote anayapata kwako.
8. Pima
thamani ya mteja ya muda mrefu.
Kuna wateja ambao wananunua
mara moja na kuondoka na kuna wateja ambao wataendelea kununua kwako kwa muda
mrefu. Wateja wanaonunua mara moja na kuondoka unaweza kupata faida kubwa,
lakini ndio imeishia hapo. Wateja ambao wananunua muda mrefu unaweza kupata
faida ndogo, ila utaendelea kuipata kwa muda mrefu. Jua wateja wale wa muda
mrefu na endelea kuwapatia thamani nzuri.
9.
Tumia mtandao wa intaneti na mitandao ya kijamii kuwa karibu na wateja wako.
Mtandao umerahisisha sana
mfanyabiashara kuwa karibu na wateja. Hakikisha biashara yako ipo kwenye
mtandao kwa kuwa na tovuti, kuwa na blogu na kuwa na kurasa kwenye mitandao ya
kijamii. Utatumia mitandao hii kutoa taarifa muhimu kuhusiana na biashara yako.
10. Toa
zawadi na motisha kwa wateja.
Kuwa na njia ambapo utatoa
zawadi mbalimbali kwa wateja wanaorudi tena kwenye biashara yako. inaweza kuwa
kuwapatia kuponi za punguzo kadiri wanavyonunua mara nyingi, au kutoa punguzo
la bei kama mteja ananunua mara nyingi. Vyovyote vile hakikisha mteja anapata
motisha pale anaponunua kwako kwa muda mrefu.
kwa ushauri wa kibiashara piga 0713735601 au email johnhmwende@yahoo.com
No comments:
Post a Comment