Rais
wa Nigeria Muhammadu Buhari ametangaza kuwa ana $150,000 (£100,000) kwenye
akaunti zake za benki, katika hatua inayolenga kuendeleza uwazi na kupiga vita
ufisadi serikalini.
Kiasi
hicho kinaonyesha kuwa amekuwa akiishi “maisha ya kujinyima”, msemaji wake
Garba Shehu amesema.
Bw
Buhari anamiliki makao matano na nyumba mbili za matope, pamoja na mashamba
kadha, akaongeza.
Kiongozi
huyo wa zamani wa kijeshi alichaguliwa kuwa rais mwezi Machi ahadi zake kuu
zikiwa kukabiliana na ufisadi na ukosefu wa usalama.
Ufisadi
ni tatizo sugu katika taifa hilo lenye uchumi mkubwa barani Afrika na mwezi
uliopita, Bw Buhari alisema $150bn (£100bn) zimeporwa kutoka kwa hazina ya
serikali.
Bw
Shehu alisema kupitia taarifa kuwa Bw Buhari ana shamba la matunda na renchi
yenye ng’ombe 270, kondoo 25, farasi watano na ndege wengi.
Pia
anamiliki hisa katika kampuni tatu - Berger Paints, Union Bank na Skye Bank,
taarifa hiyo iliongeza.
Hata
hivyo, makamu wa rais wa Nigeria Yemi Osinbajo ni tajiri kumshinda mdosi wake.
Taarifa
hiyo ilisema Bw Osinbajo ana $900,000 (£600,000) kwenye akaunti zake za benki.
Kwenye
fomu ya kutangaza utajiri wake, Bw Osinbajo pia alifichua anamiliki nyumba nne,
moja ikiwa ya vyumba viwili vya kulala ambayo analipia mkopo mjini Bedford,
Uingereza.
Taarifa
hiyo haikusema thamani halisi ya mali yote ya rais na makamu wake, ikieleza
kuwa stakabadhi zilizokabidhiwa Afisi ya Maadili zitafanywa wazi kwa umma
karibuni baada ya ukaguzi wake kukamilika.
